Nov 9, 2012

MJUE STAA WETU WA LEO!!


Akiwa ni mwenye kipaji katika kucheza kun fu, karete na michezo mingi inayofanan na hiyo kwa pamoja inajulikana kama martial arts alijifunza akiwa na umri wa miaka nane.
Alizaliwa Beijing tarehe 26 April 1963, Jet li alianza mafunzo ya kiutamaduni kwa kuingia kwenye martial arts akiwa na umri wa miaka 8. Akiwa ana umri wa miaka 11 alishinda mashindano ya kitaifa katika mchezo wa karate na miaka 8 baadae aliingia rasmi kwenye tasnia ya filamu. Filamu yake ya kwanza ilikuwa “shaolin temple” 1982.
Alitengeneza filamu nyingine “Born to defend” ambayo ilionesha uhalisia wa maisha ya binadamu ya kawaida lakini haikufanya vizuri sokoni. Li akatoa Shaolin Temple ya pili kabla hajafanya nyingine the folk hero, wong Fei – Hung  akiwa muongozaji , “Once upon a time in china” mwaka 1991. Mwaka 1992 na nyingine mbili 1993 ikiwemo “the Legend of Fong sai – Yuk” na moja 1997.
Jet li alitengeneza filamu inayoendana na filamu aliyotengeneza Bruce Lee ya “Fist of Fury” na yeye kuiita filamu yake “fist of legend” mwaka 1994. Wamarekani walianza kumfahamu alipotoa filamu iliyomtambulisha kwao ya “Lethal Weapon 4” mwaka 1998
Toka kipindi hicho alianza kuingia mikataba na Hollywood na kutoa filamu kama “Romeo must Die (2000)” “kiss of the Dragon” (2001), “Hero” (2002) “war” (2007) na Forbidden Kingdom” mwaka 2008 akiwa na Jackie Chan. Li pia alicheza “Mummy” Jomb of the Dragon Emperor mwaka huohuo
Mwaka 2010 alicheza filamu nyingine kama “ying yang” “Expendables” ambayo ilienda na kutoa Expendables 2 mwaka 2012 akiwa na wasanii wakongwe katika tasnia ya filamu Marekani Sylvester (Rambo), Bruce Wills, Arnold, Van Damme, Dolph na wengine wengi.Alioa mara mbili, mwaka 1987  alioa Huang Qiuyan na kubahatika kupata watoto wawili wa kike Si na Taimi kabla ya kuachana mwaka 1990. Mwaka 1999 alioa mke mwingine ambaye ni mwigizaji maarufu sana Nina Li Chi, waliyezaa naye pia watoto wawili Jane (2000) na Jada (2002)
Jet li alipata maafa Desember 2004, alipokuwa anamwokoa mwanae Jane katika moja ya hotel zake anazomiliki ilipotokea kimbunga cha tsunami na kubomoa jingo hilo. Ilisadikika amefariki dunia lakini yupo hai na alipona yeye na mtoto wake inga yeye aliteguka mguu na kupata majeraha madogo madogo.


Ikulu: Hatuwezi kumzuia Lissu kumshtaki Rais






SIKU moja baada ya Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu kusema atawasilisha hoja ya kumshtaki Rais Jakaya Kikwete iwapo atashindwa kuwaondoa kazini majaji wasio na sifa aliowateua, Ikulu imemwambia aendelee na mchakato wake.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema jana kuwa hakuna anayemzuia Lissu kushtaki kama anaona kuna sababu za kufanya hivyo.“Lissu ni Mbunge na ana haki zake za msingi na kama amefikia hatua hiyo anaweza kufanya hivyo... hakuna mtu ambaye anaweza kumkataza. Nani mwenye uwezo wa kuingilia uhuru wa mtu?”

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge jana, Lissu alisema amechukua uamuzi huo baada ya kuona Bunge limeikalia ripoti ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyomhoji kuhusu kauli yake ya kuwatuhumu majaji kuwa baadhi yao hawana sifa.
Alisema ameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona Rais Kikwete ambaye ana mamlaka ya kuteua majaji, ameshindwa kuwaondoa kazini majaji hao wasiokuwa na sifa.
Lissu alisema atawasilisha hoja yake hiyo kwa kutumia Kanuni ya Bunge sehemu ya 11, Ibara ya 121, 122, 123, 124, 125 na 126 na pia kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 146 A.
Sehemu ya 11 ya Kanuni ya Bunge, Ibara ya 121 inaeleza kuwa mbunge yeyote anaweza kuwasilisha kwa Spika taarifa ya hoja ya kumshtaki Rais kwa madhumuni ya kumuondoa Rais madarakani kupitia azimio la Bunge kwa mujibu wa Ibara  ya 46 A ya Katiba ikiwa inadaiwa kwamba Rais; ametenda vitendo ambavyo kwa ujumla vinavunja katiba au sheria ya maadili ya viongozi wa umma.
Lissu alisema atakusanya saini za wabunge kuunga mkono hoja yake ambayo ni asilimia 20 kwa mujibu wa Kanuni za Bunge. Wabunge wote kikatiba ni 357.
Julai 13, mwaka huu wakati akitoa maoni ya kambi ya upinzani katika Wizara ya Katiba na Sheria bungeni, Lissu alisema uteuzi wa majaji umegubikwa na ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema baadhi ya majaji walioteuliwa hawana sifa, uwezo na kwamba hawakufaa kufanya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha Bunge kuiagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Hassan Ngwilizi kumhoji ili athibitishe kauli yake.
Alisema wakati akihojiwa na kamati hiyo, pamoja na nyaraka nyingine, aliwasilisha nakala ya ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa mwaka 2008 na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kuchunguza uteuzi wa majaji nchini.
Alisema ripoti ya kikosi kazi hicho kilibaini kuwapo majaji ambao hawana sifa ya kufanya kazi hiyo, lakini Rais Kikwete ameshindwa kuwaondoa kazini.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, alisema hali ya Mahakama ni mbaya, kwani kuna majaji wawili ambao waliwahi kukamatwa kwa rushwa wakiwa mawakili, lakini wakateuliwa kufanya kazi hiyo.
Alisema baadhi ya majaji hawana uwezo hata wa kuandika hukumu kutokana na kutojua vyema lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo inayotumika katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
Alisema ili mtu aweze kuchaguliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu lazima awe na elimu ya shahada ya kwanza ya sheria, awe ametumikia miaka 10 mahakamani na anayechaguliwa kuwa jaji wa Mahakama ya Rufani lazima awe ametumikia miaka 15 mahakamani.
Mbali ya kueleza hayo, Lissu alisema kwamba alitoa pia katika kamati hiyo, ushahidi unaoonyesha kuwa kuna jaji mmoja wa Mahakama Kuu ambaye hawezi hata kuandika sentensi moja ya Kiingereza ilinyooka... “Kama jaji hawezi kuandika hata sentensi moja ya Kiingereza ilinyooka, tunaweza vipi kuwa na Mahakama  inayotenda haki?”
Alisema kuna jaji mwingine ambaye ameongezewa mkataba wa kufanya kazi mara ya tatu kitu ambacho ni kinyume cha sheria. Alisema kwa mujibu wa Tume ya Mahakama, hakuna jaji ambaye anaweza kufanya kazi kwa mkataba kwa vipindi vitatu.
Kama Lissu atachukua hatua hiyo, itakuwa ni mara ya pili kwa mbunge kuwasilisha bungeni hoja ya kutaka kumwajibisha kiongozi wa juu serikalini.
Mara ya kwanza alikuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe katika Bunge lililopita alipokusanya saini za wabunge kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akitaka awawajibishe baadhi ya mawaziri waliokuwa wametajwa kuhusika katika matumizi mabaya ya madaraka katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Hata hivyo, Rais Kikwete alifanya mabadiliko makubwa katika Baraza lake la Mawaziri hivyo kuzima hoja hiyo ya Zitto.


Serikali yataja kampuni 15 zinazodaiwa kusababisha tatizo la mafuta nchini

 MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetaja kampuni 15 ambazo Serikali imedhamiria kuzifutia leseni kutokana na kushindwa kuagiza mafuta nje ya nchi na kusababisha Tanzania kukabiliwa na uhaba wa nishati hiyo.

Mbali na hilo, Serikali imeipa leseni ya kuagiza mafuta kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (COPEC) kuagiza mafuta nje ya nchi ili kukabiliana na ubabaishaji ulioonyeshwa na baadhi ya wafanyabiashara hiyo nchini.
“Ewura imezitaka kampuni 15 kujieleza kwa nini zisichukuliwe hatua kali, hata kuzifutia leseni kabisa,” alisema Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Haruna Masebu kwenye mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, jana.

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Tanga Petroleum  Ltd,  DFCG International Ltd, Mohamed Twalib Petrol Station Ltd, Petrol (T) Ltd, Amazon Petroleum, Danvic Petroleum, Petrol Sol (T) Ltd, Bright Sta Energ Co Ltd na EXCO Oil Co. Ltd.
Nyingine alizitaja Petromark Africa, Oil Link (T), Riva Oils (T) Ltd, Metrol Petroleum (T) Ltd, Afroil Investment Ltd na Swiss Singapore Overseas Ltd.
Masebu alisema licha ya Ewura kuzipa kampuni hizo leseni hazijawahi kuagiza mafuta hivyo kusababisha tatizo la upatikanaji wa mafuta hapa nchini.
“Mpaka sasa kampuni 68  za mafuta zimepewa leseni ya kuagiza mafuta nje ya nchi na  Ewura,” alisema Masebu.
Wiki tatu zilizopita, Tanzania ilikabiliwa na upungufu mkubwa wa mafuta kiasi kwamba Serikali iliamuru mafuta yaliyokuwa yasafirishwe nje ya nchi yauzwe nchini.
Hata hivyo, aliwaondoa wasiwasi Watanzania kwamba hali ya upatikanaji wa mafuta imerejea kama kawaida na kuonya wafanyabiashara kuwa watachukuliwa hatua kali ikibainika wanakula njama za kuvuruga kanuni za mamlaka.
Sambamba na hilo, Masebu alisema Ewura imeokoa Sh1.4 Trilioni baada ya kutumia mfumo wa pamoja wa kuagiza mafuta kutoka nje  katika kipindi cha Januari 2009 hadi Agosti 2012.
Alisema mpaka sasa kampuni 68 za mafuta hapa nchini zimepatiwa leseni na Mamlaka hiyo katika kuagiza na kusambaza mafuta hapa nchini.
Masebu alifafanua kuwa kupitia mfumo wa uagizaji wa pamoja (BPS) kwa siku, jumla ya lita 1.7 milioni za mafuta ya Petrol sawa na asilimia 50 zinatumika  kwa siku hapa nchini ikifuatiwa na lita 3.5 milioni za Dizeli  sawa na asilimia 49.
Aliongeza kuwa kwa upande wa mafuta ya taa jumla ya lita 200,000 sawa na asilimia 30.7 zinatumika kwa siku  hapa nchini na hivyo ni kwa mujibu wa  takwimu halisi  za matumizi ya mafuta kwa siku kutoka mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja.