Nov 9, 2012


Serikali yataja kampuni 15 zinazodaiwa kusababisha tatizo la mafuta nchini

 MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetaja kampuni 15 ambazo Serikali imedhamiria kuzifutia leseni kutokana na kushindwa kuagiza mafuta nje ya nchi na kusababisha Tanzania kukabiliwa na uhaba wa nishati hiyo.

Mbali na hilo, Serikali imeipa leseni ya kuagiza mafuta kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (COPEC) kuagiza mafuta nje ya nchi ili kukabiliana na ubabaishaji ulioonyeshwa na baadhi ya wafanyabiashara hiyo nchini.
“Ewura imezitaka kampuni 15 kujieleza kwa nini zisichukuliwe hatua kali, hata kuzifutia leseni kabisa,” alisema Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Haruna Masebu kwenye mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, jana.

Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Tanga Petroleum  Ltd,  DFCG International Ltd, Mohamed Twalib Petrol Station Ltd, Petrol (T) Ltd, Amazon Petroleum, Danvic Petroleum, Petrol Sol (T) Ltd, Bright Sta Energ Co Ltd na EXCO Oil Co. Ltd.
Nyingine alizitaja Petromark Africa, Oil Link (T), Riva Oils (T) Ltd, Metrol Petroleum (T) Ltd, Afroil Investment Ltd na Swiss Singapore Overseas Ltd.
Masebu alisema licha ya Ewura kuzipa kampuni hizo leseni hazijawahi kuagiza mafuta hivyo kusababisha tatizo la upatikanaji wa mafuta hapa nchini.
“Mpaka sasa kampuni 68  za mafuta zimepewa leseni ya kuagiza mafuta nje ya nchi na  Ewura,” alisema Masebu.
Wiki tatu zilizopita, Tanzania ilikabiliwa na upungufu mkubwa wa mafuta kiasi kwamba Serikali iliamuru mafuta yaliyokuwa yasafirishwe nje ya nchi yauzwe nchini.
Hata hivyo, aliwaondoa wasiwasi Watanzania kwamba hali ya upatikanaji wa mafuta imerejea kama kawaida na kuonya wafanyabiashara kuwa watachukuliwa hatua kali ikibainika wanakula njama za kuvuruga kanuni za mamlaka.
Sambamba na hilo, Masebu alisema Ewura imeokoa Sh1.4 Trilioni baada ya kutumia mfumo wa pamoja wa kuagiza mafuta kutoka nje  katika kipindi cha Januari 2009 hadi Agosti 2012.
Alisema mpaka sasa kampuni 68 za mafuta hapa nchini zimepatiwa leseni na Mamlaka hiyo katika kuagiza na kusambaza mafuta hapa nchini.
Masebu alifafanua kuwa kupitia mfumo wa uagizaji wa pamoja (BPS) kwa siku, jumla ya lita 1.7 milioni za mafuta ya Petrol sawa na asilimia 50 zinatumika  kwa siku hapa nchini ikifuatiwa na lita 3.5 milioni za Dizeli  sawa na asilimia 49.
Aliongeza kuwa kwa upande wa mafuta ya taa jumla ya lita 200,000 sawa na asilimia 30.7 zinatumika kwa siku  hapa nchini na hivyo ni kwa mujibu wa  takwimu halisi  za matumizi ya mafuta kwa siku kutoka mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja.

No comments: