Nov 29, 2012



POLISI AFUKUZWA KAZI BAADA YA KUMBAKA MTUHUMIWA WA KIKE


JESHI la Polisi mkoani Mbeya limemfukuza kazi askari wake Enock Daffa (22) kwa tuhuma za kufanya  mapenzi na mtuhumiwa wa kike mwenye umri wa miaka 25 katika Kituo cha Polisi cha Mji mdogo wa Tunduma, Wilaya ya Momba, mkoani hapa. 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Athuman Diwani, askari huyo alitenda kosa hilo Novemba 21,2012 na kwamba mtuhumiwa aliyefanya naye mapenzi alikuwa akikabiliwa na kosa la wizi.
 
Kamanda Athumani alisema kuwa mbali ya kufukuzwa kazi askari huyo tayari amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mbozi ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Aidha alisema kuwa hali kama hiyo haitaweza kuvumiliwa na Jeshi la Polisi na kwamba atakayebainika kufanya tukio kama hilo adhabu yake itakuwa ni kufukuzwa kazi.
 
Kamanda huyo alitoa wito kwa askari polisi kufanya kazi kwa kufuata sheria na kanuni za Jeshi la Polisi kama mwongozo unavyowaagiza ili kulinda maadili ya Jeshi la Polisi ambacho ndicho chombo kinachotumika na wananchi katika kuzisimamia sheria.
 
Akizungumzia tukio hilo, baba mzazi wa askari huyo alisema kuwa kitendo alichofaya mtoto wake si cha kiungwana ambacho pia kimetia fedheha familia yake pia kwa jeshi la Polisi ambalo limepewa dhamana ya kutunza usalama wa raia na mali zake.

MIKOPO KWA WANAFUNZI AMBAO NI WATOTO WA VIGOGO YAPIGWA MARUFUKU


BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar, imeagizwa kuacha mara moja upendeleo wa kutoa mikopo kwa watoto wa vigogo kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo.

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Sharif Hamad alitoa agizo hilo jana alipozungumza na uongozi na watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Zanzibar Mnazi Mmoja mjini hapa.

Seif alisema yapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wazazi, kwamba Bodi hiyo inatoa mikopo kwa watu ambao hawana sifa, wakiwamo watoto wa vigogo.

“Yapo malalamiko mengi ya wananchi na wazazi kuhusu Bodi hii, ikiwamo kutoa mikopo kwa njia ya upendeleo kwa watu ambao hawana sifa na watoto wa wakubwa,” alisema.

Alikumbusha watendaji wa Bodi hiyo, kwamba taasisi hiyo imeanzishwa kusaidia maendeleo ya watoto masikini wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za masomo.

“Hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, kutoa mikopo kwa watoto wa masikini wasiokuwa na uwezo wa kugharimia masomo,” alisisitiza.

Alisema wakifanikiwa kutekeleza malengo hayo kwa kiasi kikubwa, Bodi itatoa mikopo kwa wanafunzi wengi na kuepusha urasimu na kutiwa shinikizo kutoka kwa wakubwa.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Iddi Khamis alisema Bodi imezidiwa na maombi na mahitaji ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaohitaji mikopo hiyo wakiwamo wenye sifa.

Akifafanua, Iddi alisema kwa sasa vipo vyuo vya elimu ya juu vinne vikiwa na wanafunzi wenye mahitaji ya mikopo kwa ajili ya kujiendeleza zaidi, lakini Bodi haina uwezo huo.

“Tumezidiwa na idadi ya wanafunzi wanaohitaji mikopo ya elimu ya juu sasa…vipo vyuo vikuu vinne vyenye wanafunzi wanaohitaji mikopo,” alisema.

Hata hivyo, Khamis alisema kwa bajeti ya mwaka 2012/13, Bodi imeongezwa bajeti ya fedha kutoka Sh bilioni 4 hadi Sh bilioni 8 ingawa bado hazitoshi.

Alifafanua, kuwa maombi ya mikopo kwa wanafunzi yameongezeka kutoka 800 hadi 1,800 na Bodi imeshindwa kuwapa mikopo wanafunzi hao wa ziada hivi sasa.

Hata hivyo, wanafunzi wanaokosa mikopo kutoka Bodi hiyo bado wana nafasi ya kuomba kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.