Tayari rufaa hiyo imeshapangiwa jopo la majaji
watu wa Mahakama ya Rufani watakaoisikiliza na kuitolea uamuzi na
imepangwa kusikilizwa wiki ijayo.
Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufani, rufaa hiyo imepangwa kusikilizwa Desemba 7 mwaka huu.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa rufaa hiyo itasikilizwa na majaji Salum Massati, Katherine Oriyo na Nathalia Kimaro.
Rufaa hiyo ilifunguliwa Oktoba 25 mwaka huu na
aliyekuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Ubungo kupitia tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hawa Ng’humbi, aliyekuwa mlalamikaji katika
kesi ya msingi.
Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na
Jaji Upendo Msuya Mei 24, 2012, ilitupilia mbali madai ya Ng’humbi
ikisema alishindwa kuyathibitisha na badala yake, ikamthibitisha rasmi
Mnyika kuwa mbunge halali wa jimbo hilo. Hata hivyo, Ng’humbi
hakukubaliana na hukumu hiyo, ndipo akakata rufaa akiiomba hukumu hiyo
itenguliwe.
Ng’humbi anayewakilishwa na Wakili Issa Maige,
katika rufaa yake hiyo ameorodhesha hoja 10 za kupinga hukumu hiyo,
akidokeza kile anachokiona kuwa ni udhaifu katika hukumu hiyo.
Pamoja na mambo mengine, Ng’humbi anadai kuwa Jaji
aliyesikiliza kesi ya msingi na kutoa hukumu hiyo, alikosea katika
kutafsiri sheria na kupima ushahidi wa pande zote.
Ng’humbi anadai kuwa jaji alikosea kisheria na
kiukweli kwa kusema kuwa makosa yaliyobainika katika ujumlishaji na
kuhesabu kura na kusababisha kuwapo kwa kura 14,854, zisizohesabiwa
hayakuathiri matokeo ya uchaguzi.
Anadai kuwa aliweza kuthibitsha kuwapo kwa makosa
katika mchakato wa uchaguzi yaliyosababisha kuwapo kwa kura 14, 854
zisizohesabiwa na kwamba jaji alikosea kisheria na kiukweli kwa
kutokuhamishia kwa mdaiwa, jukumu la kuelezea sababu za kuwapo kwa
dosari hizo.
“Jaji alikosea kisheria na kiukweli kusema kwamba
kura 14,854, ambazo hazikuhesabiwa zilitokana na makosa ya kibinadamu,
bila kuwepo na ushahidi kuhusu hilo katika kumbukumbu za mahakama.”
Katika hoja nyingine, Ng’humbi anadai kuwa jaji
alikosea kisheria na kiukweli kwa kusema kuwa hazikutumika kompyuta
ambazo hazikuwa zimeidhinishwa na mamlaka husika katika kujumlisha na
kura.
No comments:
Post a Comment